CWT SINGIDA VIJIJINI: BAADHI YA MAKATIBU WA CHAMA CHA WALIMU NI MZIGO

 Mwenyekiti Mpya wa Chama cha Walimu Tanzania (CWT)  Wilaya ya Singida Vijijini, Joselen Kato Samwel,  akizungumza  na wajumbe wa mkutano mkuu wa chama hicho baada ya kutangazwa mshindi.
 Msimamizi wa uchaguzi huo, Katibu wa CWT, Manispaa ya Singida, Jones Madale (katikati), akitangaza washindi.
 Mwenyekiti  wa Chama cha Walimu (CWT ) Wilaya ya Singida Vijijini, Kitengo (KE), Jaha Mwemkala, akizungumza na wajumbe wa mkutano mkuu wa chama hicho baada ya kutangazwa mshindi wa nafasi hiyo.
Baadhi ya viongozi wapya wa Chama cha Walimu Tanzania (CWT) Wilaya ya Singida Vijijini, wakiwa katika picha ya pamoja na viongozi wa meza kuu mara baada ya kuchaguliwa kwenye mkutano mkuu wa chama hicho uliofanyika mkoani hapa leo.
 Baadhi ya wajumbe wa Mkutano Mkuu wa CWT waliochaguliwa katika vitengo mbalimbali wakiwa kwenye mkutano huo.
 Mwenyekiti wa Chama cha Walimu Tanzania (CWT ) Mkoa wa Singida, Aran Jumbe, akizungumza kwenye mkutano huo. Kutoka kushoto ni  Mwenyekiti  wa Chama cha Walimu Tanzania (CWT ) Wilaya ya Singida Vijijini, Kitengo (KE), Jaha Mwemkala na Msimamizi wa uchaguzi huo, Katibu wa CWT, Manispaa ya Singida, Jones Madale.


Wajumbe wa mkutano mkuu wa CWT, Wilaya ya Singida Vijijini  wakiomba dua kabla ya kuanza uchaguzi kwenye mkutano huo.
 Wajumbe wa mkutano mkuu wa CWT ndani ya Wilaya ya Singida Vijijini wakiwa kwenye mkutano huo.
 Wajumbe wa Mkutano Mkuu wa CWT wa Wilaya ya Singida Vijijini wakiwa kwenye mkutano huo.

Wajumbe wa Mkutano Mkuu wa CWT  Wilaya ya Singida Vijijini wakiwa kwenye mkutano huo.Na Dotto Mwaibale, Singida

CHAMA cha Walimu Wilaya ya Singida Vijijini kimeshauri ikiwezekana kufanyika kwa mabadiliko ya katiba ya chama hicho ambayo yatawawezesha makatibu wake wa ngazi zote kuanza kuhudumu nafasi hizo kupitia chaguzi zinazofanywa na mkutano mkuu ili kuongeza kasi ya uwajibikaji.

Ushauri huo umekuja kufuatia malalamiko mengi yanayotolewa na wanachama wa chama hicho dhidi ya baadhi ya makatibu ambao wamekuwa mizigo na kero katika utumishi wao suala linalofifisha ufanisi na kuongeza kero kwa walimu.

Akizungumza mbele ya wajumbe wa Mkutano Mkuu wa chama cha walimu nchini (CWT), Wilaya ya Singida Vijijini leo, Mwenyekiti  wa chama hicho wilayani humo, Joselen Kato Samwel alisema baadhi ya makatibu wanapaswa kujitathmini kama wanatosha kuwa ndani ya ofisi za CWT.

Samwel ambaye amechaguliwa kwa kura nyingi kuendelea kushika nafasi ya mwenyekiti kupitia mkutano huo muhimu wa kikatiba, alisema msingi wa uwakilishi kwa dhamana walizopewa ni utetezi wa haki na maslahi ya walimu.

“Changamoto nilizokutana nazo wakati natafuta kura ni hizi ‘utendaji mbovu! utendaji mbovu!…naambiwa na wanachama kwamba utendaji kwa baadhi ya makatibu wetu sio wa kuridhisha, walimu bado wanatumia mda mrefu kupatiwa huduma, lugha si rafiki na mengine mengi,” alisema

Samwel huku akionyesha kusikitishwa na changamoto hizo hatimaye alijikuta akishauri ikiwezekana kufanyika kwa mabadiliko ya taratibu zilizopo za kuwapata makatibu wa CWT badala ya kuajiriwa kama ilivyo sasa, ikiwezekana na wao waingizwe kwenye chaguzi na hatimaye kupimwa na wajumbe wa mkutano mkuu kila baada ya muda kuona kama wanatosha kuendelea kushika nafasi hizo au la.

Aidha, Samwel pamoja na kuwashukuru wanachama wa CWT kwa kumpigia kura nyingi, pia aliwahakikishia wale wote wanaostahili kupandishwa madaraja kuwa mchakato huo upo mbioni kukamilika, huku akisisitiza kwa kuwataka  ‘wakae mkao wa kula.’

Naye Mwenyekiti mteule wa CWT Wilaya ya Singida Vijijini, Kitengo cha Wanawake (KE), Jaha Mwemkala alisema pamoja na mambo mengine, kwa kushirikiana na viongozi wote waliochaguliwa watahakikisha  wanakwenda kuwatumikia walimu ipasavyo lengo likiwa ni kukabiliana na changamoto zinazowazunguka.Katika hatua nyingine, Mwemkala aliwasihi wanachama wote wa CWT nchi nzima kuhakikisha wanakuwa chachu ndani ya jamii kwenye utoaji elimu ya tahadhari ya kujikinga na mlipuko wa janga la corona, ili kwa pamoja kuliwezesha taifa kupita salama katika kipindi hiki kigumu. 


CATEGORIES
Share This

COMMENTS

Wordpress (0)
Disqus ( )