BODI YA MIKOPO ELIMU YA JUU YAHIMIZA WALIOHITIMU VYUO MBALIMBALI NCHINI WAREJESHE MIKOPO ILI IWASAIDIE WENGINE

 

Ofisa Mawasiliano Mkuu wa HESLB Veneranda Malima  akizungumza katika nahojiano maalum  wakati wa maonesho ya Nne ya NEEC Jijini ArushaBODI ya Mikopo ya Wanafunzi wa Elimu ya Juu (HESLB) imetoa wito kwa wanufaika waliohitimu katika Vyuo vikuu na Taasisi mbalimbali za Elimu ya juu nchini kurejesha Mikopo yao ili iweze kuwasaidia wengine wanaojiunga na elimu ya juu kukopeshwa.

Akizungunza wakati wa kufungwa kwa Maonesho ya Nne ya Mifuko na Programu za kuwawezesha Wananchi yaliyomalizika hivi Karibuni Jijini Arusha,  Meneja wa HESLB Kanda ya Kaskazini – Arusha Patrick Shoo amesema kuwa wahitimu wa elimu ya juu wanaweza kurejesha Mikopo yao kidogo kidogo hata kama wamejiajiri wenyewe kwenye ujasiriamali.

Amesema katika kipindi cha siku saba za maonesho hayo wameweza kukutana na wajasiriamali kadhaa waliojitokeza kwenye Banda lao na kupata taarifa za madeni yao na wengine kulipa kwa njia ya simu.

“Kwenye maonesho haya tumeweza kukutana na wadaiwa waliopo kwenye Sekta isiyo rasmi ambao ni wajasiriamali na tumeweza kuwapa taarifa za madeni yao na wengine wamelipa kwa njia ya simu”,  amesema Shoo.

Ameongeza kuwa wahitimu wengi huwa wanakaa kimya kwa kigezo cha kutokuwa na ajira huku wakijihusisha na ujasiriamali na kwamba wanaweza kujipanga katika kipato wanachopata kwa kujiwekea utaratibu wa kulipa taratibu hata kwa njia ya simu.

“Kitu kikubwa kwa wanufaika wetu ni kupata taarifa za madeni yao ili waweze kulipa taratibu kulingana na kipato chao. Hapa tumeweza kutoa  taarifa za madeni ya wahitimu  lakini pia wazazi na wanafunzi tumeweza kuwapa elimu ya namna ya kuomba mikopo kwa usahihi,” ameongeza.  

HESLB imekuwa miongoni mwa Taasisi za Serikali zilizoshiriki katika Maonesho ya Nne ya programu za uwezeshaji Wananchi kiuchumi yaliyoandaliwa na Baraza la Taifa la Uwezeshaji Wananchi Kiucumi (NEEC) kwa kushiriana na Serikali na yalifanyika kwa siku Saba jijini Arusha.


CATEGORIES
Share This

COMMENTS

Wordpress (0)
Disqus ( )