BODI YA MAJI BONDE LA KATI YATOA MAAGIZO MAZITO KWA WAMILIKI WA MABWAWA TOPE SUMU

 Afisa wa Maji Bonde la Kati, William Mabula, akizungumza na waandishi  wa habari (hawapo pichani) mara baada ya kukagua athari za mafuriko kufuatia kujaa kwa maziwa ya Kindai, Munang na Singidani mkoani hapa jana.

Afisa Maendeleo ya Jamii Mwandamizi,  Bodi ya Maji  Bonde la Kati, Nelea Bundala, akionesha athari za mafuriko hayo.

Muonekano wa Ofisi ya Bodi ya Maji  Bonde la Kati mkoani Singida.

Na Waandishi Wetu, Singida

KUFUATIA mvua kubwa za masika zinazoendelea kunyesha Bodi ya Maji Bonde la Kati imewataka wamiliki wote wa mabwawa yote ya tope sumu kuhakikisha wanadhibiti maji kuweza kusambaa kwenye mazingira kwa kuweka miundombinu thabiti, ikiwemo kuboresha miundombinu iliyopo ili kutoruhusu maji yenye sumu kufika kwa wananchi.

Akizungumza na waandishi  wa habari mkoani hapa jana, mara baada ya kukagua athari za mafuriko kufuatia kujaa kwa maziwa ya Kindai, Munang na Singidani, Afisa wa Maji Bonde la Kati, William Mabula, alisema kwa yeyote atakayekaidi agizo hilo atachukuliwa hatua kali.

“Wamiliki wote wa mabwawa ya maji na yote ya tope sumu hakikisheni  mnadhibiti maji kuweza kusambaa kwenye mazingira kwa kuweka miundombinu thabiti  ili kutoruhusu maji yenye sumu kufika kwa wananchi,” alisema Mabula.

Aidha, Mabula aliwataka wananchi wote wakiwemo wamiliki wa mabwawa ya maji na mabwawa ya tope sumu kuchukua tahadhari kwa kuzingatia matangazo ya utabiri wa hali ya hewa yanayoendelea kutolewa kuhusu mvua hizo zinazoendelea kunyesha kwa kasi kote nchini.

Alisema mvua hizo zinaweza kusababisha mabwawa kujaa maji zaidi ya uwezo wake hivyo kutishia usalama wa wananchi, mali zao na mazingira kwa ujumla. Kujaa kwa mabwawa hayo kunaweza kusababisha yakapasuka au kutiririsha maji katika mikondo isiyo rasmi na madhara yake yanaweza kuleta mafuriko katika vijiji, barabara, madaraja, na kuharibu miundombinu mingine.

Pamoja na mambo mengine, Afisa huyo aliwashauri kwa kuwakumbusha wamiliki wote wa mabwawa ya maji kusafisha utoro wa maji, kuimarisha tuta la bwawa kwa kuondoa miti yenye mizizi, na vichuguu juu ya tuta, kuziba matoleo yote yanayotumika kutolea maji wakati wa kiangazi na kutunza uoto wa asili ili kudhibiti uingizaji wa mchanga kwenye bwawa, ikiwemo kupanda mimea au miti rafiki ya kupunguza kasi ya kuingiza michanga kwenye bwawa.

Aidha aliwatahadharisha wananchi wote wanaoishi chini ya utoro wa maji wa mabwawa na wale wanaoishi kuzunguka migodi kuchukua tahadhari ya kupata mafuriko kutokana na kipindi hiki mabwawa mengi kujaa maji zaidi ya uwezo wake.

“Lakini kwa mujibu wa sheria nawakumbusha wamiliki wote wa mabwawa kuwasilisha mipango ya usalama wa mabwawa na mafuriko kwa Mkurugenzi wa Rasilimali za Maji ili kukabili dharula itakayoweza kutokea kutokana na mvua za masika zinazoendelea kunyesha,” alisema  Mabula
CATEGORIES
Share This

COMMENTS

Wordpress (0)
Disqus (0 )