Bilioni 100 kusambaza umeme mitaa inayofanana na vijiji

Serikali kupitia Wizara ya Nishati, imetenga Sh
103.8 kwa ajili ya kusambaza umeme  kwenye mitaa inayofanana na vijiji
mkoani Lindi.

Hayo yameelezwa na waziri wa Nishati Dk. Medard
Kalemani juzi wakati wa uzinduzi wa mradi wa usambazaji wa miundobinu ya gesi
asilia majumbani mkoani Lindi uliofanyika katika Kata ya Mnazi Mmoja 
Manispaa ya Lindi.

Kalemani amekiri kuna maeneo ya mjini ambayo
mengi yaliitwa kama mitaa na si vijiji wakati kuna mitaa ambayo haina tofauti
na vijiji.

“Tumeshatoa maelekezo kuwa mitaa yote
inayofanana na vijiji iwe kwenye miji, Manispaa ama majiji yote ipelekewe umeme
kwa Sh 27,000,” amesema.

Aidha, amesema fedha hizo zimetengwa katika
bajeti ya mwaka 2019/2020 huku akimsisitiza Meneja wa Shirika la Umeme nchini
(Tanesco) Kanda ya kusini, Feisian Makota kuzingatia na kuanza kutekeleza
maagizo hayo kuanzia Julai Mosi mwaka huu.

Awali akimkaribisha Waziri wa Nishati kuzungumza
na wananchi, Mkuu wa Mkoa wa Lindi, Godfrey Zambi alimuomba waziri huyo
kuangalia namna ya kuwaunganisha wananchi wanaoishi katika maeneo hayo sawa na
wale wa vijijini ambako miradi ya REA inatekelezwa.

Zambi alisema kuna baadhi ya mitaa ndani ya
manispaa hiyo ipo vijijini ambayo kuna haja ya Serikali kuwaangalia wananchi wa
maeneo hayo walipie malipo ya umeme sawa na yale yanayofanywa na wananchi wa
vijijini ambako miradi ya REA imefika.

CATEGORIES
Share This

COMMENTS

Wordpress (0)
Disqus (0 )