BENKI YA NMB YATOA MSAADA WA VIFAA TIBA, MADAWATI IKUNGI MKOANI SINGIDA

 Meneja wa Benki ya NMB Kanda ya Kati, Nsolo Mlozi 
(wa pili kulia) akimkabidhi Mkuu wa Wilaya ya Ikungi, Edward Mpogolo moja ya kitanda kati ya vitano na vifaa tiba vyenye thamani ya sh.milioni 5 vilivyotolewa na Benki ya NMB kwa ajili ya Kituo cha Afya cha Kata ya Iyumbu mkoani Singida jana. Kutoka kulia ni Meneja Mahusiano wa Kanda Biashara na Serikali wa benki hiyo, Peter Masawe, Meneja wa benki hiyo, Wilaya ya Ikungi, Osward Kayuni na  Mganga Mkuu wa Wilaya ya Ikungi, Katalyeba Vitalis.
 Wananchi wa Kata ya Iyumbu wakiwa kwenye hafla ya kupokea vifaa hivyo.
 Wananchi wa Kata ya Iyumbu wakiwa kwenye hafla ya kupokea vifaa hivyo.
 Wananchi wa Kata ya Iyumbu wakiwa kwenye hafla ya kupokea vifaa hivyo.
 Watumishi wa Idara ya Afya wa Halmashauri ya Wilaya ya Ikungi wakiwa kwenye hafla hiyo.
 Meneja wa benki hiyo, Wilaya ya Ikungi, Osward Kayuni akizungumza katika hafla hiyo.
 Wananchi wa Kata ya Iyumbu wakiwa kwenye hafla ya kupokea vifaa hivyo.
 Mganga Mkuu wa Wilaya ya Ikungi, Katalyeba Vitalis, akisoma taarifa fupi ya kituo hicho cha afya.

 Mkuu wa Wilaya ya Ikungi, Edward Mpogolo, akihutubia katika hafla. Kutoka kulia ni Meneja Mahusiano wa Kanda Biashara na Serikali wa benki hiyo, Peter Masawe, Meneja wa benki hiyo, Wilaya ya Ikungi, Osward Kayuni na Meneja wa Benki ya NMB Kanda ya Kati, Nsolo Mlozi.

 Meneja wa Benki ya NMB Kanda ya Kati, Nsolo Mlozi akimkabidhi Mkuu wa Wilaya ya Ikungi, Edward Mpogolo moja ya vitanda hivyo.
 Mkuu wa Wilaya ya Ikungi, Edward Mpogolo, akikabidhiwa madawati.
 Vitanda vikikabidhiwa.
 Mkuu wa Wilaya ya Ikungi, Edward Mpogolo, akimfunika shuka mkazi wa kata hiyo Flora Paul ambaye alikuwa akizindua moja ya vitanda kwa staili ya kulala.
Picha ya pamoja na mgeni rasmi Mkuu wa Wilaya ya Ikungi, Edward Mpogolo. 

 

Afisa Elimu wa Kata ya Ntuntu, Kitila Mkumbo akitoa shukurani baada ya kupewa msaada wa madawati.

 Mkazi wa kata hiyo,  Flora Paul akishukuru baada ya kupokea msaada huo.
 Katibu wa Umoja wa Wanawake wa Chama Cha Mapinduzi (UWT) wa Kata ya Iyumbu, Wilikista Ochien’g, akishukuru.
  Mkazi wa kata hiyo, Mpinya Shaha, akishukuru baada ya kupokea msaada huo.


Na Dotto Mwaibale, Singida.

MKUU wa Wilaya ya Ikungi mkoani Singida, Edward Mpogolo amewataka wajawazito katika Kata ya Iyumbu wilayani humo kujenga tabia ya kuhudhuria kliniki baada ya kusogezewa kituo cha afya.

Mpogolo alitoa ombi hilo jana wakati akipokea vifaa tiba vyenye thamani ya sh.milioni 5 vilivyotolewa na Benki ya NMB kwa ajili ya Kituo cha Afya cha Kata ya Iyumbu.

“Wakina mama sasa mmesogezewa huduma za afya na leo Benki ya NMB imewaletea msaada wa vifaa tiba jengeni mazoea ya kwenda kliniki ili kufanyiwa uchunguzi wa afya zenu mnapokuwa wajawazito” alisema Mpogolo.

Alisema hapa nchini kuna benki zaidi ya 49 zikiwepo na ndani ya Mkoa wa Singida lakini ni benki ya NMB pekee ndio imeonesha upendo na kuwa pamoja nao kwa kuwapelekea vifaa tiba hivyo.

Mpogolo alisema benki hiyo sio kwamba wana fedha nyingi la hasha lakini imewapelekea msaada huo pamoja na madawati ya kukalia wanafunzi wa Shule ya Msingi Ntuntu yenye thamani ya sh.milioni 5 jumla ikiwa ni sh.milioni 10.

Alisema benki hiyo hata katika kipindi cha ugonjwa wa Covid 19 ilitoa msaada na pia Serikali ilipotaka gawio kwa ajili ya shughuli za maendeleo ilitoa zaidi ya sh.bilioni 10.

“Niishukuru sana Benki ya NMB kwa kuunga mkono jitihada za Mhe. Rais wetu Dkt.John Magufuli za kuwaletea maendeleo wananchi” alisema Mpogolo.

Alisema mwanadamu akiwa na afya njema  anaweza kushiriki shughuli mbalimbali za maendeleo na ndio maana benki hiyo imeliona hilo na kuwapelekea msaada huo.

Aidha Mpogolo alisema katika kipindi kifupi ambacho Rais Magufuli amekuwa madarakani ameweza kujenga zaidi ya Hospitali 67, Vituo vya Afya na Zahanati zaidi ya 400 na kwa Wilaya ya Ikungi wamepata vituo vya afya viwili cha Kata ya Ihanja kilichojengwa kwa sh.milioni 500 pamoja na vifaa tiba vya zaidi ya sh.milioni 300 na kituo cha afya cha Kata ya Sepuka cha sh.milioni 400 pamoja na vifaa tiba vyenye thamani ya zaidi ya  milioni 200.

Mpogolo alitumia nafasi hiyo kuuomba uongozi wa benki hiyo kufungua tawi katika kata hiyo ambayo ndio chanzo kikubwa cha mapato ya wilaya hiyo ili kuwasaidia wananchi kuweza kuweka fedha zao badala ya kwenda makao makuu ya wilaya hiyo au Singida mjini ambako kuna umbali wa kilometa zaidi 165 na wanapo kuwa njiani kwenda kuziweka wanakuwa na wasiwasi wa usalama wao na fedha zao.

Meneja wa benki hiyo Kanda ya Kati, Nsolo Mlozi  akikabidhi msaada huo alisema benki hiyo wakati wote  imekuwa ikisaidia shughuli za maendeleo hapa nchini ikiwa ni kuunga jitihada za Rais Magufuli za kuiletea nchi maendeleo.

Alisema benki hiyo ina matawi zaidi ya 230 nchi nzima lakini katika Kanda ya Kati wanamatawi takribani 25 ambapo alimwagiza meneja wa benki hiyo Wilaya ya Ikungi, Osward Kayuni kuhakikisha anapata wakala katika kata hiyo ya Iyumbu ili kuwapunguzia wananchi changamoto ya kutunza fedha zao.

Mlozi alitaja vitu walivyotoa msaada katika kata hiyo mbali ya vitanda vitano; vitatu vikiwa vya kawaida na viwili vya kujifungulia, vifaa tiba seti moja vya kujifungulia, magodoro na madawati pia walitoa  mashuka 18 vyote vikiwa na thamani ya sh.milioni 10.

Mlozi alisema benki hiyo itaendelea kuunga mkono jitihada za Serikali kwa kuchagiza maendeleo mbalimbali hapa nchini.

Mganga Mkuu wa Wilaya ya Ikungi, Katalyeba Vitalis alisema kituo hicho cha afya kimeanza kutoa huduma rasmi Julai 20 mwaka huu kwa wakazi zaidi ya 11,000 wa kata hiyo ambao wanatoka katika vijiji vitatu.

Alisema Halmashauri ya Wilaya ya Ikungi kupitia Mkurugenzi wake Justice Kijazi ilitoa sh.milioni 1.5 kwa ajili ya kukarabati jengo la muda la kukodi lengo likiwa ni kupanua wigo wa utoaji huduma za afya kwa wananchi wa Kata ya Iyumbu iliyopo pembezoni mwa wilaya hiyo ambao walikuwa wakitembea umbali mrefu hadi Mgungira na Singida mjini kufuata huduma za afya.

Alisema halmashauri hiyo imetoa jumla ya sh.milioni 4 kwa ajili ya kulipia jengo hilo la kukodi na kuwalipia pango watumishi watatu wa kituo hicho.

Alisema kituo hicho ni cha muda kwani wanatarajia kupata sh.milioni 500 kutoka Serikalini kwa ajili ya kujenga kituo cha afya cha kudumu. 


Meneja wa benki hiyo, Wilaya ya Ikungi, Osward Kayuni aliwaomba wananchi na wafanyabiashara katika kata hiyo na vijiji jirani kujitokeza kwa wingi kufungua akaunti kwenye benki hiyo kubwa hapa nchini ambayo huduma zake zimesogezwa jirani na wananchi.

Wananchi wa Kata hiyo Mpinya Shaha, Flora Paul na Wilikista Ochien’g waliishukuru Serikali na benki hiyo kwa kuwapelekea kituo hicho cha afya na msaada huo.
CATEGORIES
Share This

COMMENTS

Wordpress (0)
Disqus ( )