Kamishna msaidizi wa Ardhi mkoa wa Arusha Geofrey Mwamsojo leo, Alhamisi Aprili 25.2024 amemrejeshea kiwanja na kumkabidhi hati mama mjane aliyetambulika kwa jina la Arafa Mohammed mkazi wa...., jijini Arusha ambaye takribani miaka 15 amekuwa akifuatilia haki yake baada ya kudhulumiwa na mtu mmoja aliyemtaja kwa jina la Alex Mtinange naye akiwa ni mkazi wa jijini humo

Akizungumza na wanahabari wakati wa kukabidhi hati hiyo Kamishna Mwamsojo amesema mama huyo ambaye marehemu mume wake alikuwa raia wa kigeni alifikisha malalamiko hayo mbele ya Waziri wa Ardhi, Nyumba na Maendeleo ya makazi Jerry Silaa alipoendesha kliniki ya ardhi jijini Arusha hivi karibuni ambapo alieleza kuwa marehemu mume wake alijenga nyumba kwenye kiwanja hicho na walikuwa wakiishi wote kama familia lakini baada ya muda mume wake alianza kuugua, na katika harakati za kupigania uhai wake alimpeleka kumuuguza kwenye nchi mbalimbali huku nyumbani akimuacha binti yake

Hata hivyo baada ya mume wake aliyekuwa raia wa... kufariki, mwaka 2012 mama huyo ambaye kiasili ni mzaliwa wa Tanga alifika kwenye nyumba hiyo lakini katika hali isiyokuwa ya kawaida alimkuta mtu tofauti akiishi, na alipofuatilia ndipo alipoelezwa kuwa nyumba hiyo kwa sasa inamilikiwa na Alex Mtinange ambaye inatajwa kuwa alikuwa kwenye mahusiano ya kimapenzi na binti yake

Inaelezwa kuwa awali wawili hao (binti wa mama huyo mjane na mpenzi wake Alex Mtinange) walikuwa wakiishi wote kwenye nyumba hiyo lakini baadaye waliingia kwenye mgogoro uliopelekea binti huyo kukimbilia nchini Kenya na ndipo Mtinange alipotumia nafasi hiyo kwa kushirikiana na Mwenyekiti wa serikali ya mtaa kujimilikisha kinyume cha sheria

Jitihada mbalimbali ambazo zilichukuliwa na mama huyo ili kurejesha nyumba yake ziligonga mwamba, hadi hivi karibuni jambo hilo lilipotua kwenye meza ya Waziri Silaa aliyetoa maelekezo kwa Kamishna msaidizi wa Ardhi mkoa wa Arusha kufuatilia na kuhakikisha mama huyo anapata haki yake, jambo ambalo limefanikiwa, ingawa nyumba iliyokuwa imejengwa ilikuwa imebomolewa na hivyo kubaki kiwanja pekee

Akizungumza baada ya kukabidhiwa hati hiyo mama huyo ametoa shukrani kwa serikali kupitia Waziri Silaa na Kamishna Mwamsojo kwa kumpigania kuhakikisha anapata haki yake, hata hivyo ametoa wito kwa viongozi na watendaji mbalimbali wa serikali nchini kuiga mfano wa viongozi hao wa kuhakikisha mara zote wanasimamia haki za wananchi ambao wengi wao wamekuwa wakizihangaikia kwa muda mrefu bila mafanikio 

Katika hatua nyingine Kamishna msaidizi wa Ardhi mkoa wa Arusha Geofrey Mwamsojo amesema atahakikisha anamaliza migogoro yote ya ardhi iliyoko mkoani humo, na kwamba ndani ya siku 90 alizopewa na Mkuu wa mkoa wa Arusha Paul Makonda kuhakikisha anamaliza migogoro hiyo anaamini atafanikisha, kwa kuwa kinachofanywa na ofisi hiyo kwa sasa si kuzalisha migogoro mipya bali kushughulikia migogoro ya zamani jambo ambalo linaendelea kwa kasi.






 


Wakala wa Huduma za Misitu Tanzania - TFS umetoa msaada wa kiasi cha shilingi 20,000,000/= kwa ajili ya kusaidia waathirika wa mafuriko Wilaya za Rufiji na Kibiti mkoani Pwani.

Akipokea msaada huo mapema hivi  leo Mei 25, 2024 Mkuu wa Mkoa wa Pwani, Mhe. Abubakar Kunenge ameshukuru TFS kwa kujali wananchi wakati huu wa changamoto ya mafuriko yaliyosababishwa na mvua zinazoendelea.

 "Fedha hizi zitatumika katika kutoa huduma kwa wananchi wanaopitia changamoto ya mafuriko Rufiji na Kibiti na ninaamini hiki mlichofanya kitaenda kutusaidia mbele kuhakikisha mazingira yanatunzwa,” alisema Mhe. Kunenga

Meneja Uhusiano wa TFS Johary Kachwamba akizungumza kwa niaba ya Kamishna wa uhifadhi Prof. Dos Santos Silayo, amesema TFS inatoa pole kwa waathirika wa mafuriko kwa maeneo mbalimbali nchini ikiwa ni pamoja na Rufiji na Kibiti,

"TFS ina misitu yenye hekta 32,902 ndani ya wilaya ya Rufiji, hivyo wana Rufiji ni Wahifadhi wenzetu na tutaendelea kuwashika mkono kipindi hiki cha changamoto ya mafuriko" Johary.

 



Na Mapuli Kitina Misalaba

Ofisi ya mkuu wa Wilaya ya Shinyanga kwa kushirikiana na viongozi mbalimbali, wadau na wananchi leo asubuhi Aprili 25,2024 wamefanya usafi wa mazingira na kupanda miti 650 katika eneo la Hospitali ya Manispaa ya Shinyanga ikiwa ni sehemu ya maadhimisho ya Miaka 60 ya muungano wa Tanganyika na Zanziber.

 Mgeni rasmi katika shughuli ni katibu tawala wa Wilaya ya Shinyanga Bwana Said Kitinga akimwakilisha mkuu wa Wilaya ya Shinyanga.

Pamoja na mambo mengina Bwana Kitinga ameikumbusha jamii kuendelea kupanda miti katika maeneo yao kama sehemu ya kukabiliana na mabadiliko ya tabia nchi.

Pia ametoa wito kwa watanzania kuendelea kushikamana na kushirikiana ili kuendeleza amani na usalama nchini.

Amesema ni vema watanzania kuendelea kushikamana  na kushirikiana katika shughuli mbalimbali za maendeleo ili kuendelea kuimarisha umoja na usalama wa taifa.

Afisa maliasili na mazingira wa Manispaa ya Shinyanga Ezra Manjerenga amesema miche ya miti 650 imependwa leo kama sehemu ya maadhimisho ya miaka 60 ya muungano wa Tanganyika na Zanziber ambapo amesema zoezi hilo ni endelevu.

Kwa upande wake Mganga mfawidhi wa Hospitali ya Manispaa ya Shinyanga Dkt. Pierina Mwaluko ameahidi kuisimamia miti hiyo ili iweze kuleta matokeo chanya.

Baadhi ya wananchi na viongozi mbalimbali ambao wameshiriki shughuli ya upandaji miti wameeleza wataendelea kuunga mkono kampeni ya upandaji miti katika jamii ambapo pia  wameahidi kuendeleza amani na umoja wa  taifa hili.

Ofisi ya mkuu wa Wilaya ya Shinyanga kwa kushirikiana na viongozi mbalimbali, wadau na wananchi imefanya usafi wa mazingira na kupanda miti katika Hospitali ya Manispaa ya Shinyanga ikiwa ni sehemu ya maadhimisho Miaka 60 ya muungano wa Tanganyika na Zanziber.

Kauli mbiu ya maadhimisho Miaka 60 ya muungano wa Tanganyika na Zanziber Mwaka huu inasema “TUMESHIKAMANA, TUMEIMARIKA KWA MAENDELEO YA TAIFA LETU”.

TAZAMA PICHA HAPA CHINI Shughuli ya upandami miti ikiendelea katika eneo la Hospitali ya Manispaa ya Shinyanga leo Aprili 25,2024 ikiwa ni sehemu ya maadhimisho ya Miaka 60 ya muungano wa Tanganyika na Zanziber.